Jaji Mkuu Martha Koome, ametoa wito kwa mawakili wapya walioapishwa hivi karibuni kutumia mafunzo yao ya kisheria kufanikisha upatikanaji wa haki na uzingatiaji wa maadili katika taaluma yao.
Koome aliwahimiza mawakili hao kutumia ujuzi wao kuinua jamii, kulinda katiba kupanua upatikanaji wa haki na kupeleka huduma za kisheria kwa Wakenya wote, hususan wale wasiojiweza katika jamii na wale wa maeneo yaliyotengwa.
Akizungumza Jumatatu wakati wa hafla ya kuwaapisha mawakili wapya, Jaji huyo Mkuu alionya dhidi ya uwakilishi hafifu na uliojitenga akiwakumbusha mawakili hao kwamba katika kila faili ya kesi kuna mapambano ya kweli ya kibinadamu kama vile wajane wanaopigania haki yao ya umiliki au wakenya wanaojitetea dhidi ya unuyanyasaji.
Koome alitoa wito wa uwakilishi wa kisheria wenye huruma katika mfumo wa kisheria akiwataka mawakili hao kukumbatia maadili ya kina ili kudumisha uaminifu kwenye taaluma yao chini ya katiba.
Aidha, aliwahimiza kukumbatia mifumo ya upatanishi na ile ya njia mbadala ya upatikanaji wa haki katika kutatua mizozo badala ya kufuata mkondo mrefu wa mahakama.