Eddy Kenzo apatanisha D Star na Mudra D Viral

Wasanii hao wawili wamekuwa wakivutana kuhusiana na hakimiliki na mgao wa mirabaha kutokana na wimbo wao maarufu Hoozambe Remix.

Marion Bosire
2 Min Read
Eddy Kenzo

Mwanamuziki wa Uganda Eddy Kenzo ameingilia kati kutatua mgogoro unaoendelea wa hakimiliki na mgao wa mirabaha kati ya D Star na Mudra D Viral kuhusu wimbo wao maarufu Hoozambe Remix.

Mgogoro huo ulikuwa umetawala mitandao ya kijamii kwa wiki kadhaa baada ya D Star kumshutumu Mudra kwa madai ya kupata zaidi ya shilingi milioni 140 za Uganda kupitia mapato ya YouTube kutoka kwenye remix hiyo, huku yeye akidaiwa kupata sehemu ndogo sana kutoka kwenye mradi huo.

Hata hivyo, Mudra alikanusha madai hayo na kusisitiza kwamba bado hajarejesha fedha alizowekeza katika kutangaza na kusambaza wimbo huo.

Eddy Kenzo alichapisha video kwenye majukwaa yake ya TikTok na Facebook akithibitisha kuwa suala hilo sasa limetatuliwa baada ya wasanii hao wawili kuafikia makubaliano.

Kulingana na Kenzo, kutokuelewana kulitokana na mkanganyiko kuhusu umiliki wa haki za msingi za wimbo pamoja na taarifa zisizo sahihi kuhusu mapato yaliyotokana na majukwaa ya kidijitali.

“Tulipata wataalamu wanaoelewa masuala ya usambazaji wa muziki, wakaangalia majukwaa yake na kugundua kuwa hajapata hata asilimia 2 ya fedha zinazodaiwa,” alisema Kenzo.

Kenzo pia alifichua kuwa wasanii hao wawili sasa wamesaini makubaliano rasmi ya maandishi yanayoeleza jinsi mirabaha ya wimbo huo itakavyogawanywa kuanzia sasa.

Aidha, alieleza kuwa D Star na Mudra wanatarajiwa kuungana tena na kuendelea kutumbuiza wimbo huo pamoja jukwaani baada ya kutatua tofauti zao.

Kenzo alisema sio jukumu lake kuweka wazi maelezo ya mkataba huo hadharani, akiongeza kwamba uamuzi wa kufichua yaliyomo utabaki kwa wasanii hao wawili iwapo wataamua kufanya hivyo.

Share This Article