Meli ya kwanza ya Kenya iliyo na bidhaa ambazo hazitozwi ushuru, imewasili nchini China leo Jumanne.
Kulingana na Wizara ya Uwekezaji, Biashara na Viwanda, bidhaa hizo zinaashiria mwanzo wa upatikanaji wa soko kwa bidhaa za Kenya, chini ya mpango wa China unaolenga kupiga jeki bidhaa kutoka Afrika na kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na Mataifa ya Afrika.
Katibu wa Biashara Regina Ombam, amesema hatua hiyo ni ishara ya ukuaji wa biashara ya pande mbili kati ya Kenya na China na kuiweka Kenya katika nafasi nzuri ya kuwa mshirika muhimu wa uwekezaji Afrika.
“Mpango huu unawakilisha fursa mpya kwa wakulima, watengenezaji bidhaa na wauzaji bidhaa nje ya nchi wa Kenya, kupanua biashara zao katika mojawepo wa soko kubwa zaidi duniani,” alisema Ombam.
Kulingana na Taasisi ya Taifa kuhusu Takwimu (KNBS), mauzo ya bidhaa za Kenya nchini China, yalipungua hadi shilingi bilioni 16.9 kutoka shilingi bilioni 26.3 mwaka 2024.
Katika juhudi za kusawazisha biashara Afrika, China ilizundua mpango wa kutotoza ushuru bidhaa kutoka Afrika mnamo Mei 1, 2026, huku ikilenga nchin 54, Kenya ikiwemo.