Rais El Sisi kuhudhuria kongamano la Africa Foward Nairobi

Msemaji wa Rais El Sisi alisema kwamba kongamano hilo linalenga kuimarisha ushirikiano kati ya Afrika na Ufaransa.

Marion Bosire
1 Min Read

Rais wa Misri Abdel Fattah El-Sisi ameondoka jijini Cairo leo, akielekea Kenya kuhudhuria kongamano la ushirikiano kati ya Kenya na Ufaransa almaarufu Africa Foward Summit linaloandaliwa leo na kesho jijini Nairobi.

Msemaji wa Rais El Sisi alisema kwamba kongamano hilo linalenga kuimarisha ushirikiano kati ya Afrika na Ufaransa kwa kuzingatia changamoto za ukuaji wa uchumi, mageuzi ya kidijitali, nishati, na marekebisho ya mfumo wa kimataifa wa kifedha, pamoja na kujumuisha vipaumbele vya Afrika ndani ya mifumo ya uchumi wa dunia.

Mkutano huo utashuhudia ushiriki mpana wa viongozi wa Afrika, Rais wa Ufaransa, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, na wakuu wengi wa mashirika ya kimataifa na ya kikanda ya kifedha, pamoja na wawakilishi wa sekta za biashara za Afrika na Ufaransa.

Balozi Mohamed El-Shenawy, msemaji rasmi, aliongeza kuwa Rais atatoa hotuba ya Misri wakati wa mkutano huo, na pia atafanya mikutano kadhaa ya pande mbili na viongozi wenzake wa Afrika pamoja na maafisa wa mashirika ya kimataifa pembeni mwa mkutano huo.

Wahusika wakuu wa kongamano hilo akiwemo Rais wa Ufaransa Emanuel Macron tayari wako humu nchini.

Share This Article