Hellen Lukoma atoa wimbo mpya

Aliomba mashabiki wake wa muziki radhi akisema amekuwa akiangazia kazi yake nyingine ya uigizaji.

Marion Bosire
2 Min Read

Hellen Lukoma mwanamuziki wa Uganda ametoa wimbo mpya baada ya kukaa kimya kwa muda sasa.

Akizungumza na wanahabari wakati wa maandalizi ya video ya wimbo huo mpya uitwao ‘Brand’, Lukoma alisema kwamba ameacha mashabiki wake wa muziki bila burudani.

Huku akiomba msamaha kwa mashabiki hao, mwimbaji huyo alisema kwamba alikuwa anaangazia kazi yake nyingine kama mwigizaji lakini sasa ana kazi mpya kwa ajili yao.

Lukoma alifafanua kwamba yeye no msanii wa muziki na wa uigizaji na ana uwezo wa kushika yote mawili sawa. “Nimekuwa kwenye runinga na nimekuwa nikitoa muziki pia na kila shabiki atachagua kazi yangu anayotaka kuunga mkono,” aliongeza.

Mrembo huyo anayeigiza kama Patra kwenye kipindi “The Hostel” na kama Hellen Mutungi kwenye “Beneath The Lies” alisomea shahada ya biashara katika chuo kikuu cha Makerere.

Alijipatia umaarufu alipokuwa katika kundi la muziki lililosambaratika la Obsessions, kabla ya kuingilia uanamitindo na uigizaji. Filamu ya kwanza ya matukio halisi aliyoigiza inaitwa Situka ya mwaka 2015 na aliigiza kama Amanio.

Hellen Lukoma aliigiza kama mwigizaji mgeni katika makala ya tatu ya kipindi cha runinga cha ‘Reserved’ cha mwaka 2013 na akaigiza pamoja na Flavia Tumusiime katika “Beneath the lies” mwaka 2014.

Alizaliwa na kulelewa jijini Kampala, nchini Uganda na ndiye kitindamimba wa watoto 6.

Share This Article