Waziri Murkomen aridhia ombi la Embarambamba

Mwanamuziki huyo alikuwa ameomba kukutana na waziri Murkomen kupitia video aliyochapisha.

Marion Bosire
1 Min Read

Waziri wa Usalama wa Ndani na Utawala wa Kitaifa Onesmus Kipchumba Murkomen, hatimaye ameridhia ombi la mwanamuziki kutoka Kisii Christopher Nyangwara Mosioma, maarufu kama Embarambamba.

Embarambamba aliandaa video inayomwonyesha akicheza kwenye matope kama kawaida yake huku akiita jina la Waziri Murkomen akitaka kukutana naye.

Leo asubuhi waziri aliridhia ombi hilo na kukutana naye katika afisi yake.

“Tunaendelea kuunga mkono tasnia ya ubunifu kwa sababu ni kitovu kikuu cha ajira kwa vijana wengi na ni chombo muhimu cha kuchochea mabadiliko chanya katika jamii,” aliandika Waziri Murkomen alipochapisha picha za mkutano huo wa leo.

Alisema kwamba alifurahia kukutana na msanii huyo ambaye pia ni mchekeshaji akitaja nguvu na uwezo wake wa kuvutia umati kote nchini kuwa vitu ninavyomfanya awe sauti ya kipekee ya kitamaduni nchini.

“Nilimhimiza Embarambamba kutumia talanta zake pamoja na ushawishi alionao kushabikia maadili mema, kupambana na dawa za kulevya na kukuza moyo wa umoja katika jamii zetu,” alimalizia Murkomen.

Embarambamba anafahamika na wengi kwa vituko vyake anapokuwa jukwaani kutumbuiza pale ambapo huwa anaruka kwa njia ambayo wengi hudhania ni hatari kwake.

Anajulikana pia kwa maneno ya ajabu anayotumia kwenye nyimbo zake ambayo mara nyingi huleta dhana tofauti na ile anayokusudia.

Share This Article