Serikali yatakiwa kuwafidia wamiliki wa nyumba zinazobomolewa

Tom Mathinji
1 Min Read
Mwenyekiti wa Taasisi ya Masoroveya nchini Eric Nyadimo, kwenye mkutano na wanahabari.

Huku serikali ya Kenya inapotekeleza ubomozi wa mijengo iliyo kwenye maeneo ya kingo za mito, Taasisi ya Wanasoroveya ya Kenya (ISK), imetoa wito kwa serikali kuwafidia kikamilifu wamiliki wa mali walioathiriwa na ubomozi huo, hususan ikiwa ujenzi ulikuwa umeidhinishwa na halmashauri husika.

Rais wa ISK Eric Nyadimo, huku akilaani uvamizi na uharibifu huo wa mali alitoa wito wa kuwepo uwiano kati ya utunzi wa mazingira na haki za mali, haki ya kijamii na uzingatiaji wa sheria.

Kwenye mkutano na wanahabari siku ya Jumanne, mwenyekiti huyo alisema ISK iko tayari kushirikiana na kundi la Kiufundi linalojumuisha asasi mbali mbali, Serikali za Kaunti, na jamii zilizoathiriwa kuhakikisha uwekaji mipaka unafanywa kwa njia halali.

Taasisi ya ISK imsisitiza kuwa umuhimu wa hatimiliki za ardhi na mipaka lazima iheshimiwe.

Kadhalika, taasisi hiyo ilitoa wito wa mbinu jumuishi katika azma ya kulinda, kudumisha na kutumia hifadhi za ardhi zilizo kando ya mito humu nchini.

Huku ikitekeleza ubomozi wa mijengo hiyo, serikali imekariri kuwa, hatua hiyo inalenga kuhifadhi mazingira na kukabiliana na mafuriko ambayo yameshuhudiwa wakati wa msimu wa mvua.

Share This Article