Kenya na Tanzania zimetia sahihi mikataba minane ya ushirikiano baina ya mataifa hayo mawili.
Marais William Ruto wa Kenya na Samia Suluhu Hassan wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wameshuhudia kusainiwa kwa makabuliano hayo katika sekta mbalimbali Jumatatu jioni jijini Dar es Salaam.
Akihutubu Rais Samia aliahidi kuharakisha mchakato wa kuondoa vikwazo vya kibiashara kwa mataifa yote mawili ifikiapo Juni 30 mwaka huu, ilivyoelekezwa na kongamano la 25 la Jumuia ya Afrika Mashariki.
“Tumezungumza kufanya vizuri kwenye mipaka yetu, kuongeza ulinzi, kuongeza umakini kwenye mipaka yetu ili watu waovu wasiwe wanavuka kufanya uovu upande wowote ule kati ya nchi zetu mbili.”akasema Rais Samia
Mikataba hiyo iliyosainiwa ni katika sekta za kawi,usafiri wa baharini,usafiri,utalii,usalama ,kilimo na viwanda.


Akizungumza baada ya kusainiwa kwa mikataba hiyo Rais Ruto alisema miradi ikiwemo ujenzi wa kituo cha kusafisha mafuta cha Tanga nchini Tanzania kutafungua fursa nyingi kwa raia wa mataifa yote mawili.
“Licha ya changamoto zilizojitokeza, uhusiano wetu wa pande mbili umeendelea kuwa thabiti ukijikita katika malengo yetu na ustawi wa pamoja.” akasema Rais Ruto
Ruto alikariri kumuunga mkono Rais Samia katika miradi itakayochangia ustawi wa ukanda huu.
Rais Ruto alimpongeza mwenyeji wake kwa kujitolea kuondoa vikwazo vya kibiashara.