Mwanamitandao wa Kenya Sammy Odhiambo maarufu kama Sammyro alidhihirisha furaha ya kipekee alipotua jijini London nchini Uingereza ambako yuko pamoja na mwenzake Arap Uria kwa ajili ya kuzuru timu ya Chelsea.
Katika video za pamoja ambazo watengeneza maudhui hao wa mitandaoni walichapisha, Sammyro alionekana akipiga magoti na kuishika ardhi ya huko huku Uria akionyesha vazi la kipekee alilounda kwa ajili ya safari hiyo.
Wawili hao wanaofahamika kwa kuunga mkono Chelsea inayoshiriki ligi kuu ya soka nchini uingereza walipata fursa ya kuzuru eneo la mazoezi la timu hiyo la Cobham walikokutana na wachezaji.
“Ninahisi kila kitu. Asante kwa kuamini kijana kutoka Maringo. Kutoka Eastlands hadi West London,” aliandika Sammyro kwenye mitandao ya kijamii.
Sammyro wakati mmoja alionekana akimfunza Mfaransa Malo Gusto mtindo fulani wa densi kutoka Kenya ambapo alionekana kushindwa mara ya kwanza lakini baadaye akang’amua hali iliyozua kicheko cha furaha.
Wakenya hao walikuwa na muda sawia na mlindalango Robert Sanchez, ambaye pia alifunzwa densi ya Kenya.
Walizuru chumba cha kubadili mavazi cha Chelsea wakazingira sare za Alejandro Garnacho na kumsemea dua kutokana na kudorora kwa mchezo wake katika siku za hivi karibuni.
Huku hii ikiwa mara ya kwanza kwa Sammyro ktagusana na wana Chelsea, Arap Uria kwa upande mwingine alipata fursa hiyo mwaka jana.