Wanahabari wa mitandaoni Tanzania watakiwa kususia mashoga

Waziri Makonda alisema habari hizo huvutia ufuasi mitandaoni lakini ni hatari kwa maadili ya taifa.

Marion Bosire
2 Min Read

Wanahabari wa mitandaoni nchini Tanzania, wamehimizwa kususia habari za watu wanaodhihirisha hulka za kishoga, wanapotekeleza kazi zao.

Wito huu ulitolewa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, jana Jumapili Mei 3, 2026 jijini Dodoma alipoongoza uzinduzi rasmi wa afisi za shirika la wanahabari hao JUMIKITA.

“Lazima kwenye Wizara yetu tuwe tunabeba taswira ya mapambano ya mmomonyoko wa maadili isiwe sisi tunaongoza kuharibu maadili ya Taifa letu, sisi ndio kioo,” alisema Waziri Makonda.

Waziri huyo aliwaomba wanahabari hao wa mitandaoni kutorudi nyuma akisema, “Sitojisikia vizuri kuona mwanamtandao wa JUMIKITA anaitwa na Bodi ya Ithibati au TCRA kisa amevunja maadili”.

Makonda alisema anafahamu kwamba wanahabari hao wa mitandaoni hupenda kuchapisha habari za watu wenye tabia za kishoga, kwani hua zinachochea ufuasi mkubwa lakini akatahadharisha kwamba wanaharibu kizazi cha kesho.

Jumuiya ya Wanahabari wa Mitandao ya Kijamii Tanzania, JUMIKITA, ilibuniwa mwaka 2021, kwa lengo la kujenga jamii ya wanahabari wenye uwezo wa kutoa habari sahihi, haraka, na kwa uwajibikaji mkubwa.

Inalenga pia kuhakikisha kwamba wanahabari wa mitandao ya kijamii wanatambuliwa na kuwezeshwa kiuchumi.

Uwezo wa jumuiya hiyo ulidhihirika hivi maajuzi wakati Madam Rita wa Bongo Star Search, BSS alionekana kumdharau na kumdhalilisha mwanahabari wa mitandaoni.

JUMIKITA ilitishia kususia kazi za Madam Rita hadi aombe msamaha hatua ambayo tayari amechukua.

Share This Article