Mwanamuziki wa mtindo wa Rap nchini Uganda Gravity Omutujju, sasa anatishia kuchukua hatua za kisheria dhidi ya mwanamuziki mkongwe nchini humo Bebe Cool kwa kukosa kumlipa.
Gravity, ambaye alihusika pakubwa kwenye mikutano ya kampeni ya Rais Yoweri Museveni mwanzo wa mwaka huu, anasema alitumbuiza kwenye mikutano kadhaa ya kampeni katika sehemu mbali mbali za nchi ikiwemo kampeni iliyopatiwa jina la “Unstoppable”.
Lakini hadi sasa, anadai kwamba, hajapokea malipo ya kazi aliyofanya, hata ingawa wana makubaliano ya kimkataba na Bebe Cool ambaye wakati huo alikuwa amesimamia masuala yote yanayohusiana na wasanii yakiwemo malipo.
Omutujju alifichua hayo wakati akiwa mubashara kwenye mtandao wa TikTok, ambapo alionekana kukatishwa tamaa na kucheleweshwa huko kwa malipo, akionya kwamba huenda akatafuta usaidizi wa kisheria, iwapo suala hilo halitatatuliwa.
“Sijalipwa hata ingawa nilitia saini mkataba na Bebe Cool. Nilitumbuiza kwenye mikutano ya kampeni ya NRM na sikuwahi kupokea malipo,” alisema msanii huyo.
Aliongeza kusema pia kwamba anadai malipo mengine ya shilingi milioni 15, pesa za Uganda kutoka kwa kampeni ya Unstoppable, akitishia vile vile kuchukua hatua za kisheria kuhusiana na hilo.
Msanii huyo anasisitiza kwamba anatarajia malipo kamili kwa kazi ya kutumbuiza ambayo alifanya.
Kampeni hiyo ya Unstoppable, ilianzishwa na vijana wa kizazi cha Z almaarufu Gen Z mwaka jana, kwa lengo la kuwasikiliza vijana wenzao na kurejesha ripoti kwa Rais Museveni.