Rais Ruto kuhutubia bunge la Tanzania

Kikao hicho kitaandaliwa Jumanne Mei 5, 2026 kuanzia saa tano asubuhi

Marion Bosire
1 Min Read
Rais William Ruto

Rais wa Jamhuri ya Kenya, William Samoei Ruto, anatarajiwa kuhutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania siku ya Jumanne, Mei 5, 2026. 

Hatua hiyo itakuwa sehemu ya ziara inayotajwa kuwa ya kuimarisha ushirikiano na Undugu wa kihistoria kati ya Kenya na Tanzania.

Tangazo hilo limetolewa leo Jumatano Aprili 29, 2026, Bungeni Jijini Dodoma na Naibu Spika wa Bunge, Daniel Sillo mara baada ya kumalizika kwa kipindi cha maswali na majibu na kusema kuwa hotuba hiyo itaanza majira ya saa tano asubuhi.

Akizungumza wakati wa kutoa tangazo hilo Naibu Spika alisema tukio hilo ni muhimu na la kihistoria ambalo pia litafuatiliwa na Viongozi Wakuu wa Kitaifa na linalenga ushirikiano wa Kindugu kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Kenya.

Mei 5, 2021, Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan alihutubia kikao cha pamoja cha bunge nchini Kenya ambapo alitumia lugha ya Kiswahili.

Rais Samia aliandikisha historia ya kuwa Rais wa kwanza wa kike kuwahi kuhutubia bunge la Kenya, wakati alikuwa katika ziara ya kikazi ya siku mbili.

Marais wa zamani wa Kenya akiwemo Uhuru Kenyatta waliwahi kufanya ziara za kikazi nchini Tanzania wakiwa madarakani lakini hatua hii ya Rais Ruto kuhutubia bunge ni ya kipekee.

Share This Article