Mwanaharakati na mchekeshaji Eric Omondi ametangaza ujio wa toleo jingine la tiketi za tamasha yake ya kuhamasisha vijana kujisajili kama wapiga kura “Tuko Kadi”.
Tamasha hiyo haina ada ya kiingilio bali kila anayetaka kuhudhuria ni sharti ajisajili na kupokea tiketi kupitia mtandao na awe na kadi yake ya kupigia kura. Akisema awamu ya pili ya utoaji tiketi itaandaliwa Jumatano wiki hii.
Zikiwa zimesalia siku tano tu kabla ya kuandaliwa kwa tamasha hiyo ya kipekee, Omondi amehimiza wanaopanga kuhudhuria tamasha hiyo wajisajili kama wapiga kura waliko na kuchukua tiketi mtandaoni.
Hata hivyo alifichua kwamba maafisa wa tume huru ya uchaguzi na uratibu mipaka watakuwepo langoni kwa ajili ya kusajili watakaofika bila kadi lakini Omondi anahimiza kujisajili mapema badala ya kwenda kupanga foleni langoni siku hiyo.
Kulingana naye, wanamuziki zaidi ya 58 tajika wa Kenya watatumbuiza kwenye tamasha hiyo itakayoandaliwa Jumalipi Mei 3, 2026 saa mbili asubuhi hadi saa 12 jioni katika bustani ya Uhuru.
Kampeni ya “Niko Kadi” imekuwa ikiendelea miongoni mwa vijana na imekuwa ikiendeshwa kupitia mitandao ya kijamii ambapo wengi wamejisajili kushiriki uchaguzi ambao ni haki yao ya kikatiba.