Rais Ruto ahimiza mageuzi ya sekta afya yanayoongozwa na Afrika

Alikuwa akizungumza katika ufunguzi rasmi Mkutano wa Kikanda wa Afya wa mwaka 2026 jijini Nairobi.

Marion Bosire
2 Min Read
Rais wa Kenya William Ruto.

Rais wa Kenya, William Samoei Ruto leo amefungua rasmi Mkutano wa Kikanda wa Afya wa mwaka 2026 jijini Nairobi.

Alitoa wito wa mabadiliko makubwa kuelekea suluhisho za afya zinazoongozwa na Afrika.

Katika hotuba yake kuu, Ruto alisisitiza kuwa Afrika sio mshiriki wa pembeni tena bali ni nguzo kuu inayounda sera za afya, ubunifu na utoaji wa huduma.

Alisema kwamba kufanyika kwa mkutano huo barani Afrika kwa mara ya pili kunaonyesha kuongezeka kwa ushawishi wa bara hili katika mijadala ya afya duniani.

Rais alibainisha kuwepo kwa pengo kubwa la usawa, akieleza kuwa Afrika inabeba zaidi ya asilimia 25 ya mzigo wa magonjwa duniani lakini inatumia chini ya asilimia 3 ya matumizi ya afya.

Kiongozi huyo alionya pia kuhusu utegemezi mkubwa wa dawa na chanjo kutoka nje, akitaja hali hiyo kuwa “isiyoweza kudumu.”

Ruto alielezea hatua zilizopigwa na Kenya katika kuboresha sekta ya afya, ikiwemo utekelezaji wa huduma za afya kwa wote kupitia Mamlaka ya Afya ya Jamii.

Tangu 2024, zaidi ya Wakenya milioni 30 wamejisajili, hatua iliyopanua upatikanaji wa huduma za afya kwa kiasi kikubwa.

Uwekezaji katika afya ya jamii, ukiwa na zaidi ya wahamasishaji wa afya 100,000 na mifumo ya kidijitali, umeboresha utoaji wa huduma na uwajibikaji.

Alihimiza kuongezwa kwa ufadhili wa ndani, kuimarishwa kwa utengenezaji wa dawa barani Afrika na uwekezaji katika rasilimali watu kwenye sekta ya afya.

Pia alisisitiza umuhimu wa maandalizi dhidi ya vitisho vipya vya kiafya kama magonjwa yasiyoambukizwa na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Akihitimisha, aliwataka washirika wa kimataifa kushirikiana kwa usawa na kwa muda mrefu, akisisitiza kuwa Afrika yenye afya ni muhimu kwa utulivu na ustawi wa dunia.

Share This Article