Gor Mahia wametanua pengo la alama sita dhidi ya wapinzani AFC Leopards, baada ya kuwashinda bao moja kwa bila katika derby ya 99 ya Mashemeji, iliyochezwa Jumapili katika uwanja wa kitaifa wa Nyayo.
K’ogalo wanaowinda taji ya 22 ya Ligi Kuu ya Kenya wamepata ushindi huo kupitia kwa bao la dakika ya 85, lililopachikwa kimiani na nahodha Alpha Onyago .
Ilikuwa njia murua ya kulipiza kisasi baada ya Leopards ukipenda Chui ama Ingwe, kushinda duru ya kwanza ya derby hiyo bao lilo hilo moja kwa nunge.
Gor wanaongoza ligi kwa pointi 61 ,wakifuatwa na Leopards kwa alama 55,zikisalia mechi tano msimu ukamilike.
Gor Mahia waterejea uwanjani Mei 10 dhidi ya Police FC iliyo ya tatu kwa alama 48,wakati Ingwe watakuwa wakimenyana na Mara Sugar Mei 9.
Katika matokeo mengine ya Jumapili Sofapaka wameshushwa ngazi baada ya kuambulia kichapo cha bao moja kwa bila kutoka kwa APS Bomet nao Kakamega Homeboyz na KCB wakaambulia sare ya 1-1.