Patient Bizimana arejelea muziki na ushirikiano mpya wa kimataifa

Amezindua wimbo mpya uitwao, "Ndihano," alioshirikisha Kimber Terry wa Marekani

Marion Bosire
2 Min Read

Mwimbaji wa nyimbo za injili nchini Rwanda Patient Bizimana amerejelea muziki baada ya kukaa kimya kwa muda, na ushirikiano mpya wa kimataifa.

Bizimana anayeishi Marekani anaonekana kuwa na mshawasha mpya anapounganisha Rwanda na Marekani kupitia wimbo wake mpya uitwao, “Ndihano,” ambao ameshirikisha mwimbaji wa nyimbo za kuabudu nchini Marekani Kimber Terry.

Mwimbaji huyo wa asili ya Rwanda anahisi kwamba wimbo huu ni safari ya kiroho ya pamoja iliyoundwa na imani, mabadiliko, na ustahimilivu.

Anakiri kwamba muda wake mbali na muziki haukuwa wa ghafla wala rahisi akisema, “Kujizoesha maisha nchini Marekani baada ya kuhamia huko kulihitaji uvumilivu na kujitoa, hasa alipokuwa akibeba majukumu mapya nyumbani”.

Bizimana anasema alipowasili Marekani kwa mara ya kwanza, ilimchukua muda kuzoea mfumo na alilazimika kusitisha baadhi ya mambo ili kuitunza familia yake kwani ndoa yake ilikuwa bado changa.

Licha ya mapumziko hayo, Bizimana anasisitiza kuwa muziki unabaki kuwa sehemu kuu ya utambulisho wake na wito wake.

“Habari njema ni kwamba nimerudi studio nikifanya kazi kwenye nyimbo mpya,” alisema, akionyesha imani kwamba, “kwa neema ya Mungu,” wasikilizaji wanaweza kutarajia nyimbo mpya mara kwa mara katika siku za usoni.

Ndihano ni sehemu ya albamu inayokuja ambayo kwa sasa inaandaliwa, ikiwa na usimamizi wa uandalizi kutoka kwa Mastola Music nchini Kenya.

Usaidizi wa kurekodi unatolewa Nashville na mshirika anayetambulika kama Patrick, huku mchango kutoka Rwanda ukitoka kwa Pashington—ikionyesha upeo wa kimataifa wa mradi huo.

Wimbo huo unatokana na Zaburi 42:2: “Kama ayala aoneavyo kiu maji ya vijito, ndivyo nafsi yangu inavyokuonea kiu, Ee Mungu.”

Bizimana anasema ujumbe huu unazungumzia moja kwa moja njaa ya kiroho ambayo wengi hupitia katika nyakati zisizo na uhakika.

Share This Article