Jamaa aliyetiwa mbaroni baada ya risasi kufyatuliwa wakati wa dhifa ya waandishi wa habari wanaofanya kazi katika Ikulu ya White House nchini Marekani, ametambuliwa.
Maafisa wa usalama walimtaja jamaa huyo aliyevuruga hafla hiyo ya Jumamosi Aprili 25, 2026 usiku kuwa Cole Tomas Allen wa umri wa miaka 31, kutoka eneo la Torrance, California.
Allen alitambuliwa kwanza na shirika la habari la Associated Press, ambalo lilisema lilifanya utambuzi huo kutokana na vyanzo vya maafisa wa usalama.
Matukio katika dhifa hiyo ambayo huandaliwa kila mwaka yalivurugika pale ambapo mtu mmoja alikimbilia eneo la maankuli ambapo alikumbana na risasi huku mmoja wa walinzi akisema aliona mtu huyo akiwa na bunduki.
Rais Donald Trump aliondolewa jukwaani haraka wakati afisa mmoja wa polisi aliyekuwa amevaa vazi la kumkinga kutokana na risasi alipigwa risasi lakini hali yake ikadhibitishwa kuwa imara mara moja.
Jeanine Pirro ambaye ni mwanasheria wa Wilaya ya Columbia anasema mshukiwa anakabiliwa na mashtaka mawili ya kutumia bunduki na shtaka moja la kumshambulia afisa wa serikali kwa kutumia silaha hatari.
Mamlaka zilisema alikuwa na bunduki aina ya shotgun, bastola na visu kadhaa, Jeanine akiamini kwamba alikuwa na nia ya kusababisha madhara na uharibifu mkubwa kadri ya uwezo wake.
Allen, ambaye amesajiliwa kama mpiga kura asiyependelea chama chochote, alitajwa kuwa mwalimu bora wa mwezi Desemba mwaka 2024 katika C2 Education, taasisi inayobobea katika maandalizi ya mitihani ya kujiunga na vyuo vikuu, ufundishaji binafsi na ushauri wa kitaaluma.