Rais wa Kenya William Ruto amesema mageuzi ambayo serikali yake imetekeleza katika sekta ya kahawa yamezaa matunda, huku wakulima wakinufaika kutokana na bei zilizoimarika.
Akizungumza wakati wa ziara yake katika kaunti ya Murang’a leo Jumamosi, kiongozi huyo wa nchi alidokeza kuwa bei ya kahawa imeimarika kutoka shilingi 60 miaka mitatu iliyopita, hadi shilingi 160 kwa kila kilo.
“Tumejitolea kwa wakulima wetu kuhakikisha wanapata fedha zaidi,” alisema Rais Ruto.
Alisema serikali imeweza kupata soko la watu bilioni 1.5 la bidhaa kutoka Kenya hatua inayofanikisha mauzo ya Kahawa, Majani Chai, Macadamia, Maparachichi, Maziwa na bidhaa zingine za kilimo.
“Tunajenga masoko 25 ya kisasa katika kaunti ya Murang’a kwa kitita cha shilingi bilioni 2.5. Masoko 600 ya kisasa yanajengwa kote nchini Kenya na kutimiza ahadi yettu kwa Mama Mboga na wafanyabiashara wengine ya kuwapa mazingira bora ya kufanya kazi.
Rais Ruto yuko kwa ziara ya kikazi ya siku mbili katika kaunti ya Murang’a, ambako anatarajiwa kuzindua na kukagua miradi ya maendeleo.