Pili Mwinyi: Mjumbe wa sauti anayevuka milima na bahari

KBC Digital News
6 Min Read

Na LI Mengyao, DONG Jiameng, na ZHAO Lei

Siku moja katika mwaka 2008, Pili Mwinyi alitoka Terminal 3 (T3) ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Beijing akashangaa kwa kuona ukumbi mkubwa wenye mwanga pamoja na pilikapilika za ndege zilizoruka na kushuka. Uhai na uwazi wa mji huo umekaa akilini mwake.

Wakati huo ulikuwa mwaka wa Michezo ya Olimpiki ya Beijing, na mwanamke huyu kutoka Zanzibar, akajiunga na Redio China Kimataifa (CRI) kama mtangazaji wa Kiswahili na kuanza safari yake ya karibu miaka ishirini ya maisha nchini China.

Kukumbatia Ndoto ya Mtangazaji

Pili Mwinyi alikulia Zanzibar. Alikuwa mwanafunzi mwerevu na mwenye bidii katika masomo hata aliwahi kushika nafasi ya kwanza katika mtihani wa mkoa. Kwa bahati mbaya, mama yake alifariki alipomaliza shule ya msingi, na familia yake ikaingia taabani kiuchumi. Yeye hakuwa na budi kuchagua kozi ya ualimu badala ya kozi ya sayansi aliyoipendelea kwa kuwa ualimu ndio uhakika wa kupata ajira baada ya kuhitimu.

Licha ya kukubali shingo upande, Pili alipiga moyo konde kwamba “Ukifanya kazi moja lazima iwe ndoto yako ukafanye juhudi zote”. Mwaka 2000, aliingia kwenye studio ya Sauti ya Tanzania Zanzibar (STZ) kwa mara ya kwanza. Kama ni mmoja wa watangazaji wanawake wachache wakati ule, mikono yake ilitoka jasho na miguu ilitetemeka.

Lakini kwa msaada wa msimamizi wake Nasra Mohammed, akamaliza utangazaji wake wa kwanza kwa mafanikio. Kuanzia hapo utangazaji ukawa azma yake ya kweli na kumwongoza hadi China.

“Somo la Kwanza” Ugenini

Baada ya kuishi huku Beijing, changamoto zilikuja moja baada ya nyingine. Lugha ndio pingamizi la kwanza. Katika usiku wa kwanza, yeye na mumewe walitaka kunywa chai, lakini walishindwa kuzungumza na muuzaji wa dukani, walirudi nyumbani patupu.“Tuliweka sukari kwenye maji ya moto tukanywa kama chai”, Pili Mwinyi anakumbuka.

Mshtuko mkubwa zaidi ulikuwa mwendo wa kazi. Pili Mwinyi, aliyezoea maisha ya “polepole”ya Zanzibar, alilazimika kuzoea mwendo wa haraka haraka wa wenzake wa China maana “muda ndio mali” hasa kwa kazi ya utangazaji. Kazi uliyopewa saa nane lazima imalizike kabla ya saa kumi. Yeye alikuwa hakufanya kazi kwa kompyuta. Ilimbidi afanye mazoezi ya kuchapa maneno wakati wa mapumziko ili aende sambamba na timu yake. Mwanamke huyu hakurudi nyuma hata kidogo.  Akajizoeza kidogo kidogo katika mwendo huo, na wasi wasi wake ukaondolewa.

Mvushaji wa Tamaduni za China na Afrika

Miaka ya karibuni, Pili Mwinyi ametafsiri maandishi mengi ya Kichina kama “Utawala wa China”. Alijitahidi sana kuielewesha dunia utamaduni na maarifa ya kichina. Alipotafsiri dhana za “Usasaishaji wenye sifa za Kichina” na “Uondoshaji umaskini uliolengwa”, yeye si mbadilishaji wa lugha tu, bali pia ni mvushaji wa tamaduni.

“Natamani kuwaambia marafiki zangu wa Afrika kwamba, usasaishaji wenye sifa za Kichina unamaanisha sio lazima kufuata njia ya Magharibi kikamilifu. Tunaweza kupata maendeleo kwa kulingana na hali halisi zetu na kudumisha mila zetu”Pili ameeleza. Marafiki wengi wa Afrika wameona uwezekano wa“kutomwacha nyuma mtu yeyote”katika njia ya maendeleo, na kuona kasi na imani za serikali ya China katika kutekeleza mipango. Kazi za Pili zimefanya busara za utawala wa China  zionekane na kueleweka.

Mbali na hayo, tamthilia na filamu za Kichina alizotafsiri na kuweka sauti zimeleta ushawishi mkubwa barani Afrika. Mathalani, tamthilia ya “Doudou na mama wakwe zake” imewaonyesha watazamaji wa Afrika kumbe Wachina wana migogoro ya nyumbani vile vile. Kwa kalamu ya Pili Mwinyi, furaha na huzuni za Wachina zimevuka milima na bahari na kuwaonyesha Waafrika picha halisi ya China ilivyo.

Kwa miaka 18 iliyopita, nyayo za Pili zimefika sehemu nyingi za China: Shanghai, Guangzhou, Shenzhen, Xinjiang, Tibet… lakini Beijing imebaki kuwa“maskani yake ya pili”. Mji huo uliojumuisha mambo ya kale na ya kisasa umeshuhudia mabadiliko yake binafsi kutoka ujana hadi upevu.

Katika matukio yote aliyopitia, jambo asiloweza kusahau ni kukutana na Rais Xi Jinping wa China. Kama ni mwakilishi wa wataalamu wa nje, Pili Mwinyi alipokelewa na Rais Xi mwaka 2013  wakati wa Mikutano Miwili. Hadi leo, bado anakumbuka taadhima ya ukumbini. Wakati Rais Xi aliposhika mkono wake akitabasamu, Pili Mwinyi akahisi unyenyekevu na ukarimu wa kiongozi huyo wa nchi kubwa. Si amejihisi tu urafiki wa watu wa China, bali pia amefarijika kwa kuthaminiwa mchango wake aliofanya kama ni mfanyakazi wa utamaduni.

Ujumbe kwa Vijana

Pili Mwinyi, kama ni mbobezi wa lugha, tafsiri na utangazaji, ana matumaini makubwa kwa vijana wa hivi leo katika kujifunza lugha za kigeni na mawasiliano ya kitamaduni. Anawahimiza vijana kujifunza lugha na kupanua maono yao, huku wasiache mizizi yao ya kiutamaduni.

Pili Mwinyi amesafiri kutoka Zanzibar hadi Beijing. Amekua kutoka mwanafunzi wa ualimu hadi mtangazaji mwandamizi wa Kiswahili. Ametumia sauti yake na kalamu yake kujenga daraja imara la maelewano kati ya China na Afrika. Hadithi yake haijaishia hapa. Imethibitisha na itaendelea kuthibitisha kwamba, mwanamke mwenye imani, hamasa na juhudi si anaweza kubadilisha maisha yake mwenyewe, bali pia anaweza kujenga ulimwengu kwa nguvu zake.

(Waandishi wanatoka Idara ya Kiswahili, Chuo Kikuu cha Lugha za Kigeni cha Beijing, BF

Share This Article