Ujenzi wa sehemu za chini ya ardhi na zile za juu ya ardhi za ukumbi wa dansi wa Ikulu ya Rais wa Marekani, Donald Trump, utaruhusiwa kuendelea, mahakama ya rufaa imeamua.
Mahakama ya Rufaa ya Marekani ya Wilaya ya Columbia iliagiza kusimamishwa kwa muda kwa utekelezaji wa uamuzi wa Jaji wa Wilaya ya Marekani, Richard Leon, wa kusitisha ujenzi huo baada ya utawala wa Trump kukata rufaa.
Sasa ujenzi unatarajiwa kuendelea hadi wakati kesi hiyo itasikilizwa tarehe 5 mwezi Juni mwaka huu wa 2026.
Maamuzi ya wiki hii yalikuja baada ya mahakama ya rufaa kumuagiza jaji kutafakari upya athari za usalama wa taifa za kusimamisha kazi hiyo, baada ya yeye kuzuia kwa muda ujenzi wote wa ukumbi huo mwezi Machi.
Uamuzi huo unaashiria ushindi kwa rais katika jitihada zake za kubuni upya jengo hilo la kihistoria la Marekani.
Leon alisema Alhamisi kwamba anaamini mradi huo unahitaji idhini ya Bunge, akiongeza kuwa hatua ya utawala huo kuainisha upya mipango ya ukumbi huo kama muhimu kwa usalama wa taifa, inaonekana kuwa ni njia ya kukwepa taratibu.
“Usalama wa taifa sio hundi isiyo na kikomo ya kuendelea na shughuli ambazo vinginevyo ni kinyume cha sheria,” aliandika.
Kufuatia uamuzi huo, Trump alienda kwenye Truth Social kumshutumu jaji kwa “kujaribu kuzuia Marais wa baadaye na Viongozi wa Dunia kuwa na mahali salama na pa uhakika pa mikutano mikubwa.”
“Yote haya yameunganishwa kama kitu kimoja kikubwa, cha gharama kubwa na chenye ugumu mkubwa, ambacho ni muhimu kwa usalama wa taifa na operesheni za kijeshi za Marekani!” aliandika, akiongeza kuwa sehemu ya chini ya ardhi itajumuisha makazi ya kujikinga dhidi ya mabomu na vifaa vya matibabu.