Wanasayansi katika Taasisi ya Utafiti wa Virusi ya Uganda wanatengeneza aina mpya ya mbu ambayo wanasema inaweza kusaidia kupunguza idadi ya wadudu wanaosambaza malaria nchini Uganda.
Kazi hii inafanywa chini ya mradi wa Target Malaria Uganda, utafiti unaochunguza mbinu za kijenetiki ambazo siku moja zinaweza kupunguza idadi ya mbu wa kike wanaobeba malaria.
Krystal Birungi, mshirika wa utafiti na uhamasishaji katika mradi huo, alisema lengo lao ni kupunguza kwa kiasi kikubwa utagaji wa mayai na idadi ya mbu wa kike wanaouma.
“Tunalenga kupunguza idadi ya mayai ambayo mbu hawa hutaga. Mbu mmoja anaweza kutaga hadi mayai 300 kwa wakati mmoja. Kwa hiyo tunajiuliza, badala ya kutaga mayai 300, tunaweza kufanya nini ili watage mayai 10 tu au wasitage kabisa,” alisema Birungi.
Alisema katika mahojiano kwamba timu tayari imezalisha mbu wanaozalisha takribani asilimia 90 ya madume, hatua muhimu ambayo inaweza kupunguza idadi ya mbu wa kike, ambao ndio wanaouma na kutaga mayai.
Utafiti huu unachukuliwa kuwa hatua muhimu kuelekea kwa kuunda suluhisho la kudumu na endelevu kwa tatizo linaloongezeka la mbu kutosikia dawa za kuwaua nchini Uganda.