Kiongozi wa upinzani nchini Uganda, Robert Kyagulanyi Ssentamu, ametunukiwa tuzo ya Kiongozi wa Ujasiri na Ubunifu wa mwaka 2026 na shirika la kujenga upya Demokrasia yaani Renew Democracy Initiative, RDI.
Ssentamu ambaye pia ni mwanamuziki anayejulikana sana kama Bobi Wine, alipatiwa tuzo hiyo katika hafla iliyofanyika jijini New York nchini Marekani.
Katika taarifa aliyotoa baada ya hafla hiyo, Kyagulanyi alitoa tuzo hiyo kwa raia wa Uganda walioteseka katika harakati za kuleta mabadiliko ya kisiasa.
Aliwakumbuka raia waliouawa, waliokamatwa au kupotezwa kwa nguvu, akisema kuwa kujitolea kwao hatimaye kutailetea nchi mustakabali bora. Tuzo hiyo inaangazia juhudi zake za kuendelea kutetea mageuzi ya kidemokrasia na haki za binadamu nchini Uganda.
Kyagulanyi pia aliwapongeza washindi wenzake, akiwemo John Bolton, Chrystia Freeland, na Mark Kelly, kwa mchango wao katika kuendeleza maadili ya kidemokrasia duniani.
Kundi hilo lenye mchanganyiko wa washindi linaakisi msisitizo wa taasisi hiyo katika ushirikiano wa kimataifa wa kulinda demokrasia.
Utambuzi huu unakuja wakati mvutano wa kisiasa unoendelea kushuhudiwa nchini Uganda, ambapo Kyagulanyi ameendelea kuwa mkosoaji mkuu wa serikali.
Ujumbe wake ulisisitiza uimara wa wafuasi wake na kuthibitisha tena dhamira yake ya kuleta mabadiliko ya kisiasa kwa njia ya amani.
Shirika la Renew Democracy Initiative, RDI lilisema kwamba tuzo hiyo inawatambua viongozi wanaoonyesha ujasiri na ubunifu katika kuendeleza misingi ya kidemokrasia chini ya mazingira magumu.