Mauzo ya tiketi za tamasha la Kalasha yaanza

Raia wa kigeni watatakiwa kulipa Dola 200 kwa muda wote wa tamasha huku wenyeji wakilipa shilingi 1500 kwa siku na shilingi 3000 kwa siku zote tatu

Marion Bosire
2 Min Read

Waandalizi wa tamasha la mwaka huu la Kalasha wametangaza kuanza kwa mauzo ya tiketi za tamasha hilo litakaloanza Aprili 28 hadi 30, 2026.

Katika chapisho kwenye mtandao ya kijamii, Tume ya Filamu Nchini, KFC ilitoa tovuti ya kujisajili na kununua tiketi za hafla hiyo ambayo ni, https://kalasha.kenyafilmcommission.go.ke/festivalandmarket/

Kulingana na bango lililochapishwa, raia wa kigeni watatakiwa kulipa Dola 200 kwa muda wote wa tamasha huku wenyeji wakilipa shilingi 1500 kwa siku na shilingi 3000 kwa siku zote tatu.

Chini ya maudhui “Kubuni Tamaduni: Kubuni upya usimulizi, fremu moja baada ya nyingine”, tamasha hilo litakutanisha waandaji filamu, wabunifu na wadau wengine muhimu ili waangazie mustakabali wa masimulizi ya Afrika.

Maandalizi ya tamasha hilo yanaendelea ambapo kwa sasa filamu zilizoteuliwa kuwania tuzo za Kalasha zinaonyeshwa katika ukumbi wa Anga jijini Nairobi.

Kazi hizo zinaonyeshwa pia nje ya Nairobi katika sehemu kama Nyeri katika chuo kikuu cha Dedan Kimathi, Kericho atika taasisi ya mafunzo ya kiufundi ya Chemosot na Kisumu katika taasisi ya Alliance Française.

Filamu hizo ni pamoja na Own Goal, Deafinately Heard, Spin to Loose, Safari, The Inkidongi, Lore, S.He Gets Me, The Big Sad Nairobi, Kito and Chacha: The Leader, Cards on the Table, Boda Love, Family Vacation na Makosa ni yangu.

Share This Article