Mwanamuziki wa Kenya Ali Yusuf ambaye wengi wanamfahamu kama Arrow Bwoy ameomba mashabiki zake ushauri kuhusiana na wimbo wake wa hivi punde aliomshirikisha Dufla Diligon uitwao “Sidechick”.
Arrow ambaye pia ni mume wa mwanamuziki Nadia Mukami alichapisha video kwenye mitandao ya kijamii leo akitaka kufahamu iwapo ukwel wimbo huo unakosea watu fulani heshima.
“Hamjambo natumai nyote mko salama, mimi ni Arrow Bwoy, niko hapa kwanza kuwashukuru kwa kuunga mkono kazi yetu ya hivi karibuni zaidi…” Alisema Arrow Bwoy kwenye video hiyo.
Lakini aliendelea kuzungumzia kile alichokitaja kuwa kizungumkuti kwamba amesikia tetesi kwamba anafaa kuondoa wimbo huo kwenye majukwaa ya mtandaoni kwa sababu kuna watu imekosea heshima.
“Sijui kama mimi ndio ninachizi ama kuna shida yoyote. Huu ni mradi tumewekeza kama shilingi milioni mbili, tunapozungumza kwenye YouTube tuna maoni kama elfu moja mengi yakiwa mazuri,” aliendelea kusema mwanamuziki huyo.
Aliwataka wanaohisi kwamba wimbo huo una tatizo wamfahamishe kwa kuweka maoni yao kwenye YouTube au wawasiliane naye kwa njia yoyote kumfahamisha ili aondoe wimbo huo.
Mkewe Nadia Mukami aliripotiwa kulalamikia wimbo huo wa Sidechick akisema kwamba hauna heshima kamwe.