Kamati ya Bunge la Taifa kuhusu Nishati, imesema taifa hili lina akiba ya kutosha ya mafuta, huku ikilaumu baadhi ya wafanyabiashara wa bidhaa za mafuta kwa kusababisha uhaba wa bidhaa hiyo.
Ikiongozwa na mwenyekiti wake David Gikaria ambaye ni mbunge wa Nakuru Mjini Mashariki, kamati hiyo ilisema uhaba unaoshuhudiwa katika baadhi ya sehemu za hapa nchini umesababishwa makusudi na baadhi ya wauzaji wanaohodhi mafuta.
“Tumeridhishwa kwamba taifa hili lina akiba ya kutosha ya mafuta,” alisema Gikaria kwenye mkutano na wanahabari.
Gikaria aliyasema hayo baada ya kamati hiyo kuzuru kampuni ya Kenya Pipeline pamoja na Halmashauri ya kudhibiti Nishati na Petroli Nchini (EPRA), kwa lengo la kuthibitisha hali halisi ya akiba ya mafuta hapa nchini, huku usambazaji wa bidhaa hiyo ukiathiriwa na vita vinayoshuhudiwa Mashariki ya Kati.
Hata hivyo, kamati hiyo ilielezea masikitiko yake kuwa bidhaa za mafuta haziwasilishwi kwa wakati katika vituo vya kuuza mafuta, licha ya wateja kulipia bidhaa hiyo.
“Tunapozungumza sasa, hakuna mafuta Kisii, Nyamira na Migori,” alisema Gikaria.
Katika kaunti ya Nairobi, wabunge hao walisema matanki yanahifadhi mafuta, ikiwa ni pamoja na tanki moja lililokuwa na lita milioni 10 za mafuta ya diesel na akiba ya mafuta ya petroli ya lita milioni 2.4