Msanii wa muziki nchini Kenya Wanjiru Gitu maarufu kama Fena Gitu au Fenamenal Woman amemsifia msanii mwenzake Nyashinski kufuatia onyesho lake la kipekee.
Fena alichapisha video inayomwonyesha akifurahia tamasha hilo la Nyashinski akiwa katikati ya umati wa mashabiki waliokuwa wamejitokeza.
“Nyashinski asante kwa kuchukulia sanaa yako kwa uzito mkubwa!! Zaidi ya kuwa shabiki, mimi ni mwanafunzi wa kazi yako, ubora na umahiri wa jukwaani. Ni muhimu sana kukuona katika kila hatua ya ubunifu wako. Pokea maua yako Mfalme, daima,” aliandika Fena chini ya video hiyo.
Aliendelea kwa kumwombea Nyashinski afanikishe kila kitu ambacho akili yake angavu inabuni na kikombe chake kifurike baraka.
Nyashinski aliandaa tamasha la muziki kwa jina “Showman Residency” ambalo lilihusisha maigizo jukwaani kuanzia Aprili 4 hadi 12, 2026 na limesifiwa kwa kiwango kikubwa na mashabiki na wadau wa muziki.
Mtangazaji Willis Raburu naye alisifia onyesho hilo kupitia video aliyochapisha ambapo anakumbuka jinsi msanii huyo alipanga onyesho hilo ambapo kwake ni muunganisho wa wabunifu.
Alitaja jinsi alikuwa amepanga wacheza densi, waigizaji na hata watengenezaji maudhui mitandaoni akisema “Watu tamasha la Showman ni onyesho la kipekee!” huku akiwahimiza waende kujionea.
Alimalizia kumshukuru akisema, “Nyashinski asante kwa kutuonyesha kile ambacho kujiamini na kujisukuma kunahusisha. Maisha yangu yamebadilika.”