Rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni ataapishwa rasmi kuhudumu kwa muhula wa saba mwezi ujao wa Mei.
Hii ni baada yake kuibuka mshindi kwenye kinyang’anyiro cha urais katika uchaguzi mkuu ulioandaliwa Januari 15, 2026.
Haya ni kulingana na tangazo lililotolewa na kituo cha habari cha Uganda chini ya Wizara ya teknolojia ya mawasiliano na mwongozo wa kitaifa.
“Kufuatia ushindi wake katika uchaguzi, Rais Yoweri Museveni ataapishwa Mei, 12, 2026,” lilisema tangazo hilo lililotiwa saini na Alan Kasujja, Mkurugenzi Mtendaji wa kituo hicho cha habari.
Kasujja alielezea kwamba hafla ya uapisho, itaandaliwa katika uwanja wa Kololo, chini ya maudhui, “Kulinda mafanikio, kupiga hatua kubwa ya ubora kuelekea hadhi ya kipato cha kati cha juu”.
Alisema wageni wengi kutoka sehemu mbali mbali ulimwenguni watahudhuria hafla hiyo huku kamati ya kitaifa ya maandalizi ikiongozwa na katibu wa kudumu katika afisi ya Rais Hajji Yunus Kakande ikijibidiisha katika maandalizi.
Museveni alitangazwa mshindi, kwa kiwango cha asilimia 71 ya kura zote zilizopigwa, na tume ya uchaguzi ya Uganda, Jumamosi, Januari 17, 2026, siku mbili baada ya uchaguzi.
Matokeo ya uchaguzi huo hata hivyo yamekuwa yakipingwa na wanasiasa wa upinzani nchini Uganda wakiongozwa na Robert Kyagulanyi Ssentamu almaarufu Bobi Wine, aliyewania Urais.
Alichapisha taarifa kwenye mtandao wa X akilalamikia kile alichokitaja kuwa makazi yake kuzingirwa na maafisa wa polisi ambao anadai waliharibu kamera za ulinzi na kuzuia watu kutoka au kuingia.
Bobi Wine hata hivyo aliambia umma kwamba aliweza kukwepa polisi hao na kuondoka nyumbani lakini akamwacha mkewe na wengine huko.
Siku kadhaa baadaye aliibuka mitandaoni akisema kwamba yuko ughaibuni ambako anashauriana na viongozi kadhaa kuhusu jinsi ya kuikomboa Uganda.