Mshukiwa wa ulanguzi wa dawa za kulevya afikishwa mahakamani

Winfred Nkatha alipatikana na magunia 8 ya bangi nyumbani.

Marion Bosire
1 Min Read

Mshukiwa wa ulanguzi wa dawa za kulevya Winfred Nkatha amefikishwa katika mahakama ya Malindi baada ya kukamatwa akiwa na kilo 255 za bangi katika eneo la Jimba, kaunti ya Kilifi.

Nkatha wa umri wa miaka 29, alikanusha mashtaka dhidi yake na mahakama ikamwachilia kwa dhamana ya shilingi milioni 2, ila hakupatiwa chaguo la dhamana ya pesa taslimu.

Alikamatwa baada ya oparesheni iliyomlenga iliyotekelezwa na maafisa wa kitengo cha kukabiliana na dawa za kulevya wa Malindi kwa ushirikiano na polisi wa kituo cha polisi cha Watamu.

Maafisa hao walikuwa wamepokea na taarifa sahihi za ujasusi zilizowaelekeza katika nyumba moja ya makazi kwenye barabara ya Mwatela mkabala na barabara ya kutoka Watamu kuelekea Gede.

Mshukiwa alipatikana akiwa kwenye nyumba hiyo na baada ya msako, maafisa walipata magunia manane yaliyokuwa na misokoto ya bangi iliyokaushwa .

Mshukiwa alipelekwa katika kituo cha polisi cha Watamu pamoja na bangi hiyo inayoaminika kuwa ya thamani ya shilingi milioni 7.65.

Idara ya Upelelezi wa Jinai, DCI inasisitiza kujitolea kwake kuharibu kabisa mtandao wa ulanguzi wa dawa za kulevya na kulinda jamii kutokana na athari zake.

Share This Article