Serikali imetoa wito kwa Idara ya Mahakama kuondoa agizo ambalo lilisimamisha utumizi wa mikakati iliyobuniwa ya kukabiliana na ajali za barabarani hapa nchini.
Mwezi uliopita, serikali ilibuni mikakati ya utumizi wa kamera za kuchunguza mwendo kasi wa magari barabarani, pamoja na kutozwa faini za papo hapo, na hatua kali dhidi ya madereva na wamiliki magari wanaosababisha majeraha au maafa kwa kukiuka sheria za trafiki.
Akizungumza leo Jumanne wakati wa ibada ya wafu ya wahasiriwa 16 wa ajali iliyotokea katika barabara ya Nyeri-Nyahururu iliyoandaliwa kwenye uwanja wa maonyesho ya kilimo wa Kabiru-ini , kaunti ya Nyeri, Kindiki alihimiza mahakama kukubali mikakati hiyo ya serikali itekelezwe, huku ikisubiriwa kusikilizwa na kuamuliwa kwa kesi inayopinga utekelezwaji wa mikakati hiyo.
“Ili kukaniliana na ajali za barabarani hapa nchini, serikali ilibuni mikakati kadhaa mwezi uliopita…..lakini mahakama ikatoa agizo la kusimamisha utekelezwaji wa mikakati hiyo wiki kadhaa zilizopita,” alisema Prof. Kindiki.
Wengine waliohudhuria ibada hiyo ni pamoja na Gavana wa Nyeri Mutahi Kahiga, naibu Gavana wa Nyeri Kinaniri Warui, Mwakilishi mwanamke Rahab Mukami, wabunge, wawakilishi wadi na wananchi kutoka eneo hilo.
Wiki iliyopita watu 16 walifariki huku kadhaa wakijeruhiwa kwenye ajali ya barabarani katika Barabara Kuu ya Nyeri- Nyahururu highway karibu na Chuo kikuu cha Dedan Kimathi.