Mwanamuziki wa Uganda Winnie Nwagi amelalamikia kile alichokitaja kuwa kisa cha kuogofya kilichohusisha shabiki mmoja katika tumbuizo moja hivi maajuzi.
Nwagi alitumia mitandao ya kijamii kuelezea aliyopitia siku hiyo huku akichapisha video inayoonyesha tukio hilo.
Shabiki husika anaonekana akijaribu kumpiga pambaja Nwagi kwa lazima na kumpapasa visivyo alipokuwa aielekea jukwaani kutumbuiza.
Akielezea kwa undani jinsi tukio hilo liliendelea, Nwagi alisema kwamba shabiki huyo hata alijaribu kumpiga busu na kujaribu kumtoa nguo na kulazimu walinzi wake kuingilia kati.
Mwimbaji huyo anasema tukio hilo lilimharibia kazi yake siku hiyo huku akisema ameshoka na visa vya kunyanyaswa na mashabiki wasiokuwa na heshima.
Nwagi ameonya mashabiki wenye tabia kama hiyo akisema kwamba sio kila siku ataweza kujizuia kuchukua hatua dhisi ya watu kama hao.
“Tulikuwa tumeanza vizuri … Hata nimechoka kutumia hiki kipaaza sauti kwenu mashabiki musiokuwa na heshima… Inauma!” alisema Nwagi akiongeza, “Mkiendelea kunijaribu, sitaweza kujizuia lakini nitawapa mnachostahili.”
Kisa hiki kinajiri wakati ambapo kisa wasia kimeripotiwa kikihusisha mwanamuziki Tracy Melon, ambaye alishambuliwa na shabiki wakati wa tamasha huko Mbarara.
Tracy alilazimika kukomesha tumbuizo lake na kuondoka jukwaani huku akitilia shaka usalama wa wanamuziki wanapokuwa kazini.