Sasha Vybz ambaye ni mwelekezi wa video nchini Uganda, ameonya wabunifu wenzake kuwa waangalifu kuhusiana na sheria iliyoimarishwa ya hakimiliki.
Vybz alikuwa akitoa maoni yake kuhusiana na sheria hiyo ambapo alitoa changamoto kwa wenzake kuhakikisha wanasoma na kuelewa sheria hiyo wasije wakafanya makosa makubwa.
“Kwanza ni lazima wabunifu wote waelimishwe kuhusu kilicho kwenye sheria hii, wakielewa watajipanga ipasavyo,” alisema Vybz.
Wabunifu wengi nchini Uganda wamefurahikia sheria hiyo ambayo itasaidia pakubwa kulinda kazi zao za ubunifu ambapo wengi wamekuwa wakipoteza kazi, kujipata kwenye migogoro na kukosa mapato.
Kulingana na Vybz ufahamu ni muhimu mno kuliko hata utekelezaji wa sheria hiyo.
Mwanamuziki Ragga Dee naye ameongeza sauti yake kwenye mjadala unaoendelea kuhusiana na sheria ya hakimiliki ambapo anasisitiza kwamba ni ya lazima kwa kila mmoja.
Dee alikuwa akihojiwa alipozungumzia pia ufahamu wa sheria husika akikosoa wanabiashara na wamiliki wa maeneo ya burudani wanaodhania kwamba sheria hiyo inahusu muziki wa Uganda pekee.
“Hata u[ige muziki wa Uganda au wa kimataifa, ni lazima utalipia cheti cha hakimiliki!” alisema Ragga Dee akiongeza kwamba hata huo muziki wa ughaibuni hawaumiliki ndiposa lazima waulipie.