Mchekeshaji na mwanaharakati Eric Omondi ataandaa tamasha la “Tuko Kadi” kama njia ya kupiga jeki kampeni ya vijana kujisajili kama wapiga kura ya “Niko Kadi”.
Omondi alitangaza hayo kupitia akaunti zake za mitandao ya kijamii wakati ambapo kampeni hiyo iliyoanzishwa na vijana kwa lengo la kuhimiza vijana wenzao kujisajili kama wapiga kura imeshika kasi.
Kulingana na tangazo lake, tamasha hilo litaandaliwa Mei 3, 2026 katika uwanja wa Uhuru Park Jijini Nairobi kuanzia saa 2 asubuhi hadi saa 12 jioni.
“Ni rasmi sasa!!! Tamasha la Tuko Kadi litafanyika tarehe 3 mwezi Mei huko Uhuru Park kuanzia saa 2 asubuhi hadi saa 12 jioni,” aliandika msanii huyo .
Tamasha hilo ni tofauti na matamasha mengine ambayo kwa kawaida hutoza ada ya kiingilio ambapo huko utahitajika tu kuonyesha kadi yako ya kupigia kura kabla ya kuruhusiwa kuingia.
Hata hivyo wanaotaka kuhudhuria wanahitajika kuchukua tiketi zao za bila malipo kulingana na Omondi ambaye amechapisha tovuti ya tiketi hizo.
Wasanii mbali mbali wakiwemo wanamuziki na wachekeshaji wanatarajiwa kutumbuiza watakaohudhuria hafla hiyo wakiwemo Bien, Savara, Octopizzo na Juliani.
Wengine ni Nameless, Jua Cali, Wyre, Redsan, Ssaru, Iyanii, Okello Max, Daddy Owen, Moji Short Baba, Rufftone
Jua Cali na wengine.
Vijana wameshangaza wengi mwaka huu kwa jinsi wamejitolea kushiriki haki yao ya kikatiba ya kuchagua viongozi wanaowataka kupitia uchaguzi mkuu wa mwaka ujao wa 2027, kiasi cha kuanzisha kampeni ya ‘Niko Kadi’.