Wachekeshaji Sammy Kioko na Tom Daktari wamekamatwa nje ya lango la afisi za serikali ya kaunti ya Machakos ambako walikuwa wamekwenda kudai haki wakiwa na wengine.
Mchekeshaji mwenza Nasra Yusuf ndiye alichapisha habari hizo kwenye Instagram akisema kwamba wawili hao walishambuliwa na kupigwa na maafisa wa serikali hiyo ya Machakos kabla ya kukamatwa.
Mapema asubuhi, Nasra alikuwa amechapisha video akiomba uungwai mkono kutoka kwa mashabiki kwa shughuli hiyo waliyokuwa wamepanga ya kuandamana nje ya afisi hizo za kaunti ya Machakos.
Mwanadada huyo alichapisha video inayoonyesha tukio la kukamatwa kwa Kioko mapema leo ambapo watu waliofunika nyuso zao kwa barakoa wanamnyemelea kumwangusha chini kabla ya kumkamata.
Sammy Kioko anaidai serikali hiyo ya kaunti shilingi milioni 19 ambazo ni malipo kwa huduma na bidhaa alizowasilisha hususan sare za maafisa wa usalama wa kaunti.
Kioko anasema kwamba amekuwa akidai deni hilo kwa muda bila mafanikio hadi wakati mmoja alilazimika kuomba mashabiki na marafiki usaidizi ili kupeleka dadake kwa matibabu nchini India.
Yapata siku tatu zilizopita, Kioko alichapisha kile kilichoonekana kuwa stakabadhi rasmi za Seneta wa kaunti ya Machakos Agnes Kavindu akiwasilisha kesi hiyo ya Kioko.
Kavindu anataka bunge la Seneti liingilie kati na kutatua mgogoro kati ya serikali ya kaunti ya Machakos na kampuni ya Kioko iitwayo Movata Fashions.
Seneta huyo anaelezea kwenye stakabadhi hizo kwamba kampuni hiyo ya Movata iliingia kwenye mkataba na serikali ya kaunti ya Machakos Aprili 15, 2024 naye akatekeleza sehemu yake lakini hajalipwa kufikia sasa.