Vijana wa Pep Guardiola, Manchester City, ndio mabingwa wa kombe la Carabao.
Hii ni baada ya kuwanyuka vijana wa Mikel Arteta magoli 2-o na kutwaa kombe hilo katika fainali ya kombe hilo iliyosakatwa katika uwanja wa Wembley jana Jumapili.
Magoli yote ya Man City yalitiwa kimiani na mchezaji Nico O’Reilly katika kipindi cha pili.
Hii ni mara ya tano kwa Man City kushinda kombe hilo.

Wengi wamemlimbikizia kipa Kepa Arrizabalaga kwa kutomakinika langoni na kuchangia ushinde wa Arsenal wakati Arteta naye akikoselewa kwa kutomwanzisha kipa namba moja wa timu hiyo David Raya.
Hata hivyo, vijana wa Guardiola walionekana kuudhibiti mchezo hasa katika kipindi cha pili, udhibiti uliozaa matunda kwa wao kutikisa wavu mara mbili.
Ushindi huo una maana kwamba Arsenal hawajaambulia kombe lolote tangu waliposhinda kombe la FA mnamo mwaka 2020.
Baada ya kichapo hicho, Arsenal wameelekeza shabaha kwa ligi kuu wanayoongoza kwa alama 70 baada ya kucheza mechi 31, mechi moja zaidi kuliko Man City ambao wana alama 61.
Wachambuzi wanasema ushinde wa Man City huenda ukawatia hamu zaidi ya kutaka kushinda ligi kuu zikiwa zimesalia takriban mechi nane kabla ya kukamilika kwa ligi kuu.