Hakuna sehemu ya nchi itatengwa katika miradi ya maendeleo, asema Kindiki

Martin Mwanje
1 Min Read
Prof. Kithure Kindiki - Naibu Rais

Naibu Rais Prof. Kithure Kindiki amewahakikishia Wakenya kwamba hakuna sehemu yoyote ya nchi itatengwa katika utekelezaji unaoendelea wa miradi ya maendeleo.

Amesema taifa hili linashuhudia utekelezaji wa miradi mikubwa kutokana na jitihada za serikali jumuishi ikiongozwa na Rais William Ruto.

Ameyasema hayo leo Alhamisi alipokagua miradi ya maendeleo katika eneo bunge la Ganze, kaunti ya Kilifi.

Prof. Kindiki alisema siasa tupu hazina nafasi nchini kwa sababu watu wana shauku tu katika kile kinachoboresha maisha yao.

“Tuko dhahiri katika mawazo yetu kwamba Kenya itabadilishwa tu siyo kupitia siasa tupu bali siasa za maendeleo. Vyama vya UDA na ODM vitaendelea kufanya kazi pamoja chini ya serikali jumuishi ili kuhakikisha nchi hii imeendelea,” alisema Naibu Rais.

“Rais William Ruto amehakikisha hakuna eneo la Kenya linaachwa nyuma au kubaguliwa katika masuala ya maendeleo. Maendeleo huko Nyanza, Magharibi, eneo la Kati, na Bonde la Ufa ni sawa na Pwani, Kaskazini Mashariki na Nairobi. Kila kaunti inapokea miradi sawa ya maendeleo.”

Gavana wa Kilifi Gideon Mung’aro na wabunge Kenneth Tungule (Ganze), Stanley Kenga (Magarini), John Bwire (Taveta), Obo Ruweida (Lamu Mashariki), Owen Baya (Kilifi Kaskazini) na Eric Wamumbi (Mathira) ni miongoni mwa waliokuwapo.

 

Share This Article