Taarifa ya BBC
Timu ya taifa ya Morocco imetangazwa kuwa mabingwa wa Kombe la Mataifa ya Afrika, AFCON 2025. Hii ni baada ya Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) kubatilisha matokeo ya awali ya fainali dhidi ya Senegal na kuipa ushindi wa mezani.
Awali, Senegal ilikuwa imeshinda mechi hiyo kwa bao 1-0 katika fainali iliyochezwa Januari 18 mjini Rabat, Morocco.
Hata hivyo, mchezo huo ulikumbwa na utata mkubwa baada ya wachezaji wa Senegal kususia kuendelea kucheza wakipinga maamuzi ya mwamuzi, ikiwemo kutolewa kwa penalti dakika za mwisho wakati matokeo yakiwa 0-0.
Baada ya mchezo kusimama kwa takribani dakika 17 huku hali ya taharuki ikitawala uwanjani, wachezaji wa Senegal walirejea kucheza kufuatia kushawishiwa na mshambuliaji nyota Sadio Mane. Penati ya Morocco iliyopigwa na Brahim Diaz iliokolewa na kipa Edouard Mendy kabla ya Senegal kufunga bao la ushindi kupitia Pape Gueye katika muda wa nyongeza.
Hata hivyo, Morocco iliwasilisha rufaa kwa CAF, ambayo sasa imekubaliwa.
Katika uamuzi wa kushangaza uliotolewa siku 58 baada ya mechi, bodi ya rufaa ya CAF imesema Senegal imekiuka kanuni na hivyo “inachukuliwa kuwa imepoteza mchezo huo kwa kufungwa magoli 3-0,” na kuipa Morocco ushindi pamoja na ubingwa.
CAF pia imetoa adhabu mbalimbali, ikiwemo faini dhidi ya pande zote mbili, huku baadhi ya rufaa za Morocco zikikubaliwa na nyingine kukataliwa.
Uamuzi huo unaingia katika historia kama mojawapo ya maamuzi yenye utata kuwahi kufanywa katika soka ya Afrika.