Rais Ruto achangia waathiriwa wa ajali ya Webuye

Mchango wake wa shilingi milioni 7.5 uliwasilishwa na Spika Moses Wetang’ula.

Marion Bosire
2 Min Read

Rais William Ruto jana alitoa mchango wake kwa familia za waliofariki na kwa walioumia kwenye ajali mbaya ya barabarani iliyotokea siku chache zilizopita huko Malaha, Webuye.

Mchango wa Rais wa shilingi milioni 7.5 uliwasilishwa na Spika wa Bunge la Taifa Moses Wetang’ula ambaye pia aliongoza mchango huo katika shule ya sekondari ya Sipala.

Wetang’ula naye alitoa mchango wake wa shilingi milioni moja huku wabunge na viongozi wengine waliokuwepo nao wakitoa michango yao.

Watu 16 walipoteza maisha katika ajali hiyo na wengine zaidi ya 20 wakiachwa na majeraha mbalimbali.

Spika Wetang’ula alitangaza kwamba kesho Jumatatu, kutaandaliwa ibada ya pamoja ya mazishi kwa ajili ya waliofariki mjini Webuye.

Kiongozi huyo alihakikishia familia za waathiriwa kwamba wataendelea kusimama nao hadi kila familia itakapozika mpendwa wao.

Kabla ya hapo, Wetang’ula alihudhuria mchango na ibada katika kanisa la Kanyadhiang SDA katika eneo bunge la Karachuonyo, kaunti ya Homa Bay.

Akizungumza kanisani humo, Wetang’ula aliwataka viongozi wa kisiasa wakome kupiga siasa za migawanyiko kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.

Alisema matamshi mabaya ya kisiasa yanaiweka nchi katika hatari akisisitiza kwamba mara nyingi Kenya hushuhudia nyakati za siasa zenye mvutano kwa sababu ya maneno ya wanasiasa yanayokuza chuki.

Wetang’ula alishangaa jinsi wanasiasa fulani wanajitafutia umaarufu kupitia ukabila badala ya kuhimiza umoja wa kitaifa.

Wanasiasa walihimizwa waendeshe kampeni faafu badala ya kurushiana matusi, ili kudumisha mshikamano hata baada ya uchaguzi.

Share This Article