Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja, ameonya kuwa Huduma ya Taifa ya Polisi itayaangamiza magenge yote ya wahalifu, huku taifa hili linapojiandaa kwa Uchaguzi Mkuu mwaka 2027.
Akiwahutubia Maafisa Wakuu wa Polisi katika chuo cha mafunzo kwa wafanyakazi wa serikali kaunti ya Kwale leo Ijumaa, Kanja aliwahakikishia wakenya kwamba Huduma ya Taifa ya Polisi itafanikisha mazingira ya amani wakati wa Uchaguzi Mkuu ujao.
Kanja alisema maafisa wa usalama wako macho kukabiliana vikali na wanaotishia amani kufwatia habari za kuchipuka kwa magenge ya wahalifu yanayotumiwa na wanasiasa kuzua rabsha.
Kanja alisema hayo alipokutana na Maafisa Wakuu wa Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai, kujadili mbini za kukabiliana ulanguzi wa pesa na kuzuia ufadhili kwa magaidi,miongoni mwa maswala mengine.
Mkutano huo pia ulihudhuriwa na Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mohamed Amin, na maafisa wengine wakuu wa polisi.