Mahakama Kuu imesimamisha utekelezaji wa faini za papo hapo kwa wanaokiuka sheria za trafiki, zilizoanza kutekelezwa hivi maajuzi.
Mamlaka ya Uchukuzi na Usalama Barabarani, NTSA ilianzisha utekelezaji wa faini hizo kupitia mfumo wa kielektroniki kama njia ya kukabiliana na utepetevu ambao mara nyingi husababisha ajali.
Jaji Bahati Mwamuye ametoa agizo la kukomesha utekelezaji wa faini hizo kufuatia ombi lililowasilishwa na wakili Shadrack Wambui, anayepinga uhalali wake.
Kulingana na Jaji Mwamuye, faini hizo hazitatekelezwa hadi kesi ya wakili Wambui itakaposikilizwa na kuamuliwa.
NTSA ilitangaza mwanzo rasmi wa utozaji wa faini za papo hapo kwa wanaokiuka sheria za trafiki siku ya Jumatatu Machi 9, 2026.
Ilani iliyotiwa saini na Mkurugenzi Mkuu wa NTSA ilichapishwa siku hiyo kwenye magazeti makuu ya humu nchini.
Mfumo huo unajiendesha kielektroniki na wakiukaji wa sheria za trafiki watakuwa wakipokea jumbe fupi kuhusu ukiukaji huo kwenye simu zao za rununu.
Waathiriwa wa faini hizo walikuwa wameelekezwa kuzilipa kupitia benki ya KCB katika muda wa siku saba na iwapo watakosa kulipa, pesa hizo zitakuwa zikizalisha riba.
Utozaji wa faini za papo hapo, ulikuwa kati ya mapendekezo ya ripoti ya Baraza la Kitaifa la Utekelezaji Haki, NCAJ kama njia moja ya kupunguza ajali za barabarani.
NCAJ iliandaa ripoti ambayo ilikabidhiwa Rais William Ruto aliyesisitiza utekelezaji wa mapendekezo fulani mara moja kama vile faini.