Rubani aliyefariki katika ajali na mbunge Ng’eno kuzikwa Jumamosi

Kamati ya bunge ya mazishi ya waathiriwa itatuma mwakilishi kwenye mazishi hayo.

Marion Bosire
1 Min Read

Rubani aliyekuwa akiendesha ndege iliyopata ajali na kusababisha kifo cha mbunge wa Emurua Dikirr Johana Ng’eno na wote waliokuwemo atazikwa Jumamosi hii.

Mwenyekiti wa kamati ya muda ya bunge iliyojukumiwa kusimamia mazishi ya Ng’eno na wenzake Julius Melly, ndiye alifichua hayo.

Katika mkutano wa kamati hiyo wa kujadili mazishi yaliyoandaliwa Ijumaa na Jumamosi, Melly alielekeza kwamba mwakilishi wa kamati hiyo atahudhuria mazishi ya rubani Kanali Mstaafu George Were.

Mazishi hayo yataandaliwa Jumamosi Machi 14, 2026, nyumbani kwake huko Nyakach.

Kulingana na Melly, bunge linamchukulia rubani Were kama mmoja wao kwani alihudumia wabunge kadhaa kwa miaka mingi, katika kazi yake ya kurusha ndege.

Wanachama wa kamati hiyo walikubaliana kwamba wangeandaa mkutano na familia ya Were na kuzuru familia ya Ng’eno kabla ya kuhitimisha rasmi jukumu la kamati hiyo ya muda.

Melly alimshukuru Gavana wa kaunti ya Narok Patrick Ole Ntutu na serikali ya kaunti hiyo kwa usaidizi wa maandalizi ya mazishi ya waathiriwa wa ajali hiyo ya ndege.

Serikali ya kaunti hiyo ilisimamia ada za chumba cha kuhifadhi maiti cha Lee, usafiri wa wanafamilia wa waathiriwa na kuhakikisha upatikanaji wa vifaa vilivyosaidia kuendesha shughuli hata wakati wa mvua kubwa.

Share This Article