Ripoti ya NADCO: Bunge latakiwa kupitisha miswada muhimu

Miswada hiyo inajumuisha ule wa Rasilimai za Kitaifa ya mwaka 2022 unaolenga kubuni mikakati ya ugavi sawa wa mapato kutoka kwa rasilimali za kitaifa.

Tom Mathinji
2 Min Read

Bunge limetakiwa kupitisha haraka miswada muhimu katika muda wa siku 90 zijazo, ambayo ilitokana na ripoti ya  Kamati ya  Uwiano wa Kitaifa  (NADCO).

Kwenye mapendekezo yake, kamati hiyo ilipendekeza kubuniwa kwa kamati jumuishi itakayowashirikisha  wabunge wa Bunge la Taifa na wale wa Seneti kuharakisha upitishwaji wa miswada iliyokwama.

Miswada hiyo inajumuisha ule wa Rasilimai za Kitaifa ya mwaka 2022, unaolenga kubuni mikakati ya ugavi sawa wa mapato kutoka kwa rasilimali za kitaifa kati ya serikali kuu, zile za kaunti na jamii.

Huku ikiwasilisha ripoti mbele ya mkutano wa pamoja wa wabunge wa ODM na UDA, kamati hiyo pia ilipendekeza kuwa Tume ya Kitaifa ya Kutetea Haki za Kibinadamu, KNCHR ibuni sheria zinazowalinda waandamanaji pamoja na mali kuambatana na sehemu ya 37 ya katiba.

Wakati huo huo, kamati hiyo ilitaka Mamlaka ya Kusimamia Utendakazi wa Polisi (IPOA) kukamilisha uchunguzi wake kuhusu maafisa wa polisi watundu katika muda wa miezi sita na kuchapisha matokeo yake ili kuongeza imani ya umma kwa maafisa wa polisi.

Kamati hiyo iliyokuwa ikiongozwa na Seneta mteule wa zamani Agnes Zani, ilibuniwa kuongoza utekelezwaji wa ajenda 10 zilizotokana na mkataba wa maelewano kati ya Rais William Ruto na aliyekuwa kiongozi wa ODM hayati Raila Odinga mwaka 2023.

TAGGED:
Share This Article