NTSA yaanza kutoza faini za papo hapo

Wakiukaji wa sheria za trafiki watapokea jumbe fupi kuhusu ukiukaji huo kwenye simu zao za mkononi.

Marion Bosire
1 Min Read

Halmashauri ya Kitaifa Uchukuzi na Usalama Barabarani, NTSA imetangaza kwamba imeanza rasmi kutoza faini za papo hapo kwa wanaokiuka sheria za Trafiki.

Ilani iliyotiwa saini na mkurugenzi mkuu wa NTSA ilichapishwa leo kwenye gazeti kuu za humu nchini.

Mfumo huo kulingana na ilani hiyo, unajiendesha kielektroniki na wakiukaji wa sheria za trafiki watakuwa wakipokea jumbe fupi kuhusu ukiukaji huo kwenye simu zao za rununu.

“Mfumo huu ni wa kielektroniki na unafanya kazi bila mwingilio wa binadamu, kuhakikisha uwazi, ufanisi na uwajibikaji katika utekelezaji wa sheria za trafiki.” ilielezea ilani hiyo.

Watakaoathiriwa na faini hizo watahitajika kuzilipa kupitia benki ya KCB katika muda wa siku saba na iwapo watakosa kulipa, pesa hizo zitakuwa zikihesabiwa riba.

Mmiliki wa gari ambalo litakuwa na deni la faini hataweza kufanya lolote kwenye mfumo wa NTSA hadi pale ambapo atalipa faini husika.

Waendeshaji magari sasa wanashauriwa wazingatie sheria za trafiki na kujibu haraka jumbe watakazopokea.

Utozaji wa faini za papo hapo, ulikuwa kati ya mapendekezo ya ripoti ya baraza la kitaifa la utekelezaji haki NCAJ kama njia moja ya kupunguza ajali za barabarani.

NCAJ iliandaa ripoti hiyo ambayo ilikabidhiwa Rais William Ruto aliyesisitiza utekelezaji wa mapendekezo fulani mara moja kama vile faini.

Share This Article