Rais William Ruto ambaye kwa sasa anahudhuria kongamano la viongozi wa mataifa wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, ameagiza kuhusishwa kwa maafisa mbali mbali katika kushughulikia madhara ya mafuriko.
Kiongozi huyo wa nchi aliagiza kwamba kundi hilo la maafisa wa mashirika mbali mbali litumwe nyanjani mara moja na chakula cha msaada kitolewe kwa waathiriwa.
Haya yanafuatia mafuriko ya ghafla yaliyoshuhudiwa Nairobi na maeneo mengine ya nchi Ijumaa usiku na Jumamosi asubuhi. Mafuriko hayo yalisababisha maafa na uharibifu mkubwa wa mali.
Katika taarifa, Rais alisema kwamba kundi hilo litaongozwa na maafisa kutoka wizara ya masuala ya ndani na utawala wa kitaifa kwa ushirikiano na jeshi la Kenya KDF.
Pamoja na mashirika mengine ya kushughulikia dharura, kundi hilo linafaa kushirikisha uokoaji, kusaidia waathiriwa na kuhamisha watu kutoka maeneo ya hatari.
Ruto aliagiza kundi hilo kugawia waathiriwa chakula cha msaada haraka huku serikali ikishughulikia bili za hospitali za waathiriwa waliolazwa hospitalini.
Kulingana na Rais, serikali ya kitaifa na serikali za kaunti zinashirikiana kuhakikisha ushughulikiaji mwafaka wa majanga unaotoa kipaumbele kwa usalama wa raia.
Alikiri kwamba mkasa huu wa mafuriko umeonyesha haja iliyopo ya kutafuta suluhu za kudumu kwa mafuriko katika miji, akitaja mpango wa uhuishaji wa mto Nairobi.
Takwimu za Huduma ya Taifa ya Polisi, NPC, zinaonyesha kwamba watu wasiopungua 29 waliokolewa kutokana na hatari ya mafuriko.