Serikali kuzisaidia familia za walioangamia kwenye ajali ya ndege

Watu sita, akiwemo mbunge wa Emurua Dikirr Johana Ng'eno, waliangamia kwenye ajali ya ndege katika eneo la Mosop, kaunti ya Nandi Jumamosi iliyopita.

Martin Mwanje
2 Min Read
Viongozi mbalimbali wakati wa ibada ya wafu katika kanisa la AGC mtaani Karen

Serikali itatoa usaidizi kwa familia za watu sita walioangamia kwenye ajali ya ndege katika eneo la Mosop, kaunti ya Nandi Jumamosi iliyopita, akiwemo mbunge wa Emurua Dikirr Johana Ng’eno. 

Ahadi hiyo imetolewa na Naibu Rais Prof. Kithure Kindiki leo Jumatano wakati wa ibada ya wafu iliyofanyika katika kanisa la AGC mtaani Karen jijini Nairobi.

“Tuna uwezo kama serikali kuzisaidia familia zote ili kuhakikisha hatuzitelekezi kwa sababu ya kuondokewa na wapendwa wao,” alisema Prof. Kindiki wakati wa ibada hiyo.

Alisema serikali itasimama na familia za waliofiwa wakati na hata baada ya mazishi na kuzitaka kuwasilisha mahitaji yao ili yaweze kuangaziwa.

Ibada hiyo ilihudhuriwa na Maspika Moses Wetang’ula wa Bunge la Taifa na Amason Kingi wa Seneti miongoni mwa viongozi wengine wengi wakiwemo Magavana na Wabunge.

Wetang’ula akitumia fursa hiyo kuwaonya Wakenya dhidi ya kutoa kila aina ya makisio juu ya kilichosababisha ajali hiyo.

Badala yake, ameitaka Mamlaka ya Usafiri wa Anga nchini kutathmini upya njia za kuboresha usalama wa marubaini na abiria wao wanaotumia huduma za usafiri wa anga.

Familia za waathiriwa zilitumia fursa hiyo kuelezea zilizvyoatuliwa mioyo kwa kuondokewa na wapendwa wao.

“Daima utakuwa sehemu ya maisha yangu,” alisema mjane Nayianoi Ntutu Ng’eno aliyemwomboleza mumewe wakati akivuta kumbukizi za nyakati nzuri walizokuwa nazo pamoja katika safari yao ya ndoa.

“Ni wakati wa kuhuzunisha, lakini tunashukuru kwamba tuko hapa kusherehekea maisha ya N’eno. Tunathamini urithi anaoacha na tunasherehekea maisha aliyoishi,” alisema kakaka marehemu Ng’eno, Barnabas Ng’eno, kwenye risala yake ya rambirambi.

Mazishi ya waathiriwa yamepangwa kufanyika Ijumaa hii.

Share This Article