Serikali imetangaza awamu ya mwisho ya nyogeza ya mishahara kwa Maafisa wa Polisi, wale wa Magereza na maafisa wa Huduma ya Vijana kwa Taifa (NYS).
Katibu katiba Wizara ya Usalama wa Taifa Dkt. Raymond Omollo, amesema nyongeza hiyo itatekelezwa kuanzia mwezi Julai mwaka huu, hatua hiyo ikiwa sehemu ya mpango mpana wa marekebisho katika sekta ya Usalama wa Taifa.
Kupitia kwa taarifa leo Jumatano, Omollo alisema hayo yaliafikiwa kufuatia mkutano wa kamati tekelezi ya kitaifa kuhusu marekebisho katika huduma hizo tatu, akidokeza kuwa nyongeza hiyo ya mishahara kwa muda wa miaka mitatu mfululizo, ndiyo ya juu zaidi tangu uhuru wa taifa hili.
“Maafisa wa vyeo vya chini ndio waliofaidika zaidi katika nyongeza hiyo ya mishahara, kama ilivyoagizwa na Rais William Ruto,” alisema Dkt. Omollo.
Kufuatia nyongeza hiyo ya mishshara, afisa wa polisi wa cheo cha konstebo atapokea mshahara wa shilingi 57,700, kutoka shilingi 38,975, hii ikiwakilisha nyongeza ya asilimia 48. Hii ikitekelezwa pia kwa maafisa wa idara ya magereza.
Maafisa wa cheo cha konstebo wanaofuzu watapokea mshahara wa shilingi 29,296 kutoka shilingi 20,390 kabla ya mwezi Julai mwaka 2024.
Afisa wa cheo cha chini wa Huduma ya Taifa ya Vijana (NYS), atapokea mshahara wa shilingi 26,222 huku wa juu zaidi katika cheo hicho ukiwa shilingi 37,912.
Maafisa kutoka huduma hizo tatu za usalama walianaza kupokea nyongeza ya mishahara Julai 1, 2024 kufuatia agizo la serikali.