Rais William Ruto ametangaza ujio wa mpango wa serikali wa kuweka vifaa vya kuzalisha nishati kutokana na miale ya jua katika shule kadhaa kote nchini.
Mpango huo utakaogharimu shilingi bilioni 45 utafaidi taasisi 3,200 za elimu na unalenga kusaidia kuafikia matumizi ya nishati safi na kulinda mazingira.
Kiongozi wa nchi aliyasema hayo Machi 1, 2026, alipoongoza maadhimisho ya miaka 100 ya shule ya upili ya kitaifa ya Alliance katika eneo bunge la Kikuyu.
Kulingana naye, mpango huo utasaidia taasisi za masomo kukoma kutegemea kuni na vyanzo vingine vya nishati na kuangazia matumizi ya nishati inayotokana na jua katika kupika, mwanga na matumizi mengine.
Rais Ruto alifichua kwamba mradi huo wa nishati itokanayo na jua unatarajiwa kuzalisha megawati 780 za umeme na hivyo kuinua kwa kiwango kikubwa nishati safi na kupunguza gharama ya nishati shuleni.
Majaribio ya mpango huo tayari yamefanywa na kufanikiwa katika shule 266 katika sehemu mbalimbali za nchi na sasa ni wakati wa kutekeleza mradi huo kwa shule zote.
Kuhusu nishati ya ziada itakayozalishwa wakati wa likizo, kiongozi wa nchi aliitaka Wizara ya Nishati kuhakikisha inauzwa na kujumuishwa kwenye mtandao wa kitaifa wa nishati.
Sherehe hiyo ya miaka 100 ya uwepo wa shule ya Alliance ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, wabunge, wanafunzi wa zamani na hata wa sasa miongoni mwa wengine.