Spika Wetang’ula amwomboleza Ng’eno

Mbunge huyo wa Emurua Dikirr alifariki jana na watu wengine watano katika ajali ya ndege huko Nandi.

Dismas Otuke
1 Min Read
Spika wa Bunge la taifa Moses Wetangula.

Spika wa Bunge la Taifa Moses Wetang’ula amemwomboleza mbunge wa Emurua Dikirr Johana Ng’eno, aliyefariki jana katika ajali ya ndege huko Nandi.

Katika taarifa, Wetang’ula alisema kwamba amehuzunishwa mno na kifo cha mbunge huyo ambacho alikitaja kuwa pigo kwa watu wa eneo bunge la Emurua Dikirr na taifa kwa jumla.

“Kwa niaba ya tume ya huduma za bunge, bunge la taifa na yangu binafsi, ninatoa pole kwa familia, marafiki na watu wa Emurua Dikirr kufuatia kifo cha Ng’eno, kiongozi shupavu”, aliandika Wetang’ula.

Spika huyo ambaye pia alitoa taarifa rasmi kuhusu kifo cha Ng’eno, alimsifia kwa kujitolea kwake kutetea maslahi ya watu aliokuwa akiwakilisha bungeni.

Alimtaja kuwa mtumishi mzuri wa umma ambaye kujitolea kwake katika huduma na maendeleo kulionekana wazi wakati wa uongozi wake.

Wetang’ula alisema kifo cha Ng’eno kimeacha pengo kubwa katika bunge la taifa na katika uongozi wa eneo bunge la Emurua Dikirr.

Katika taarifa rasmi, Wetang’ula alitangaza kubuniwa kwa kundi la wabunge 10 litakaloongoza mipango ya mazishi ya mwendazake kwa ushirikiano na familia yake.

Mbunge wa Tinderet Julius Melly, ataongoza kundi hilo, akisaidiwa na mwenzake wa Buuri, Mugambi Rindikiri.

Share This Article