Maafisa wa kitengo cha kukabiliana na mihadarati (ANU) mjini Mombasa, wamewakamata washukiwa sita wa ulanguzi wa mihadarati, wakiwa na bangi ya thamani ya shilingi milioni 72.
Baada ya kupokea habari za kijasusi, maafisa hao walisimamisha lori lenye nambari za usajili KDT 659G katika barabara kuu ya Mombasa-Nairobi, lililopatikana likisafirisha mihadarati hiyo.
Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) kupitia ukurasa wa X, ilisema baada ya ukaguzi wa kina, lori hilo lilikuwa na magunia 50 ya bangi yenye uzani wa kilo 2,400.
“Dereva wa lori hilo Nolden Ogola Misieba na msaidizi wake Andrew Kaida, walikamatwa papo hapo,” ilisema DCI.
Wakati huo huo, maafisa hao walinasa magari mengine mawili yanayoaminika kuwa sehemu ya usambazaji wa mihadarati hiyo, ambayo ni Toyota Noah lenye nambari za usajili KCL 458S likiendeshwa na Jefferson Kamau akiwa na mshirika wake Lawrence Onyango, Nissan Note lenye nambari za usajili KCZ 567R likiendeshwa na John Lutomia, na Toyota Vitz lenye nambari za usajili KDQ 867K likiendeshwa na Samuel Juma Okoth.
Washukiwa hao sita wanazuiliwa kwenye korokoro za polisi huku mihadarati na magari yaliyonaswa yakizuiliwa kama sehemu ya ushahidi.