Wanajeshi walioongoza mapinduzi ya serikali nchini Niger sasa wanapendekeza serikali ya mpito ambayo itaongoza nchi hiyo kwa muda wa miaka mitatu kabla ya kurejelea uongozi wa kiraia.
Wameonya dhidi ya mwingilio wowotw kijeshi wakisema haitakuwa rahisi kwa wahusika.
Jenerali Abdourahmane Tchiani, alitoa taarifa kupitia runinga Jumamosi jioni ambapo alitoa maelezo hayo lakini hakutoa taarifa zaidi kuhusu mpito.
Alisema tu kwamba wahusika wa mpito huo watatajwa katika muda wa siku 30 zijazo kwenye kikao cha mazungumzo kitakachoandaliwa na baraza la kijeshi linalotawala nchi hiyo hivi sasa.
Taarifa ya Tchiani ilijiri baada ya mkutano na wawakilishi wa shirika la kiuchumi la afrika magharibi ECOWAS jijini Niamey ambapo alifafanua kwamba baraza lake na watu wa Niger kwa jumla hawataki vita.
“Lakini acha nifafanue, iwapo tutavamiwa, haitakuwa rahisi jinsi watu wengine wanafikiria.” alisema Tchiani.
Shirika la ECOWAS limeiwekea Niger vikwazo kadhaa kwa sababu ya mapinduzi yaliyotekelezwa Julai 26, 2023 na kuagiza kuandaliwa kwa jeshi litakalojukumiwa kurejesha uongozi wa kiraia na kikatiba nchini Niger.
Nchi 11 wanachama wa ECOWAS kati ya zote 15 zimekubali kutoa wanajeshi kwa ajili ya oparesheni hiyo.
Kwenye hotuba yake ya dakika 12, Tchiani alidai kwamba ECOWAS inajiandaa kushambulia Niger kwa kuandaa kikosi kwa ushirikiano na jeshi fulani la kigeni.
Alifafanua kwamba sio nia ya baraza lake kuendelea kusalia madarakani na kwamba wako tayari kwa mazungumzo.