Msanii wa muziki nchini Uganda Eddy Kenzo amesema kwamba alijaribu kusuluhisha kile kinachoaminika kuwa ugomvi kati yake na mwanamuziki mwenza Azawi bila mafanikio.
Kenzo ambaye jina lake halisi ni Edrisah Kenzo Musuuza anasema aliomba mazungumzo ya moja kwa moja kati yake na Azawi kwenye runinga au katika uwepo wa mashahidi lakini ombi lake halikujibiwa.
Msanii huyo ambaye ni mshauri mkuu wa Rais Museveni katika masuala ya wabunifu anasema ugomvi huo sio wa kibinafsi bali unatokana na habari za kupotosha.
Kulingana naye, Azawi huenda alipatiwa habari za kupotosha kuhusu mazuri ambayo serikali imefanyia wasanii au anafanya makusudi kuyapuuza.
Disemba mwaka jana Azawi alikashifu uongozi wa Kenzo ambaye ni Rais wa chama cha kitaifa cha wanamuziki nchini Uganda – UNMF akimlaumu kwa kukosa kupigania haki za wasanii nchini Uganda.
Kulingana na Azawi, Kenzo hana athari yoyote katika tasnia ya muziki hasa katika kushabikia juhudi za mabadiliko ya sheria kuhusu hakimiliki.
Alisema Kenzo anashawishiwa na serikali na hajaelewa kabisa majukumu yake katika wadhifa wake.
Azawi alipendekeza pia mawasiliano ya moja kwa moja kati ya Rais Museveni na wasanii na kukashifu mawasiliano yasiyo ya moja kwa moja kupitia kwa mawakala kama Kenzo.